“Ni yapi mahitaji? Upendo kwa binadamu, unyoofu kwa wote, kuakisi umoja wa ulimwengu wa binadamu, uhisani, kuwashwa kwa moto wa upendo wa Mungu, kufikia ujuzi wa Mungu na kile kinachoongoza kwenye ustawi wa binadamu.”
— ‘Abdu’l‑Bahá
Dhana ya kimsingi katika mafundisho ya Kibahá’í ni kwamba utakaso wa tabia ya ndani na huduma kwa binadamu ni vipengele vya maisha visivyotengana. Shoghi Effendi, katika barua iliyoandikiwa kwa niaba yake, husema:
Hatuwezi kutenganisha moyo wa binadamu kutoka mazingira yanayotuzunguka na kusema mara tu moja kati ya hivi vimerekebishwa vyote vitakuwa vimeboreshwa. Mwanadamu ni kiumbe hai na ulimwengu. Maisha yake ya ndani huyabumba mazingira na nayo pia huathiriwa nayo kwa kina. Kimoja hutenda juu ya kingine na kila badiliko linalodumu katika maisha ya mwanadamu ni tokeo la mwingiliano huu tegemezi.
Katika mwanga huu, Wabahá’í wamekuja kuthamini uendeshaji wa kusudi lenye pande mbili ambalo ni la msingi kwa maisha yao: kushughulikia ukuaji wao wa kiroho na kiakili na kuchangia kwenye mabadiliko ya jamii .
Kusudi hilo lenye malengo mawili husaidia kuelekeza jitihada za Wabahá’í katika maeneo yote. Hivyo, kwa mfano, wanatarajiwa siyo tu kusali na kutafakari kila siku juu ya maisha yao wenyewe, bali pia kufanya jitihada kujaza mazingira yao na roho ya ibada; wanaombwa, siyo tu, kuimarisha ujuzi wao wenyewe wa Imani, bali pia kushiriki na wengine mafundisho ya Bahá’u’lláh; wanaaswa siyo tu kujifunza kupinga maamurio ya nafsi katika maisha yao wenyewe, bali pia kuweka jitihada, kwa ujasiri na unyenyekevu, kupindua mielekeo ya utamaduni unaotukuza kuendekeza nafsi na inayomomonyoa misingi ya mshikamano.